Breaking News



Tuma maoni, ushauri, habari na picha kuptia
-          machibya.richard@yahoo.com
-          Facebook Machibya Richard

WATU WATATU WASHIKILIWA NA POLISI MKOANI SINGIDA KWA KOSA LA WIZI WA PESA KWA NJIA YA MTANDAO.




 Hapo juu na picha ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida ACP Thobias G. Sedoyeka akiongea na waandishi wa habari leo Ofisini kwake.

Na. Sylvester Richard

Singida.
Jeshi la Polisi Mkoani Singida linawashikilia watu watatu wanaojihusisha na matukio ya wizi kwa njia ya mtandao.Watu hao ni Matutu s/o Ngese, (28), Muikizu, Mkazi wa Temeke DSM , Nyamoko s/o Amosi nyamoko, (27), Muikizu Mkazi Wa Kitunda Mwanagati DSM  na Matutu s/o Zakayo katyetye, (26), Mjita na Mkazi wa vingunguti - Ilala DSM.

Akiongea na waandishi wa habari leo katika Ofisi yake  Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida ACP Thobias G. Sedoyeka amesema kuwa kukamatwa kwa watuhumiwa hao kumetokana na wizi wa Tsh. 900,000/=    walioufanya kwa njia ya mtandao katika duka la M – pesa la Dianarose d/o Ngughu lililopo Katika maeneo ya Soko la Kiomboi, Kata ya Kiomboi, Tarafa ya Kisiriri, Wilaya ya Iramba ambapo siku ya tarehe 28.05.2016 majira ya 4:00 asubuhi  mmoja wa watuhumiwa  alifika dukani kwa mlalamikaji  na kutaka awekewe salio  kiasi hicho kwenda  namba 0767 – 117552. Mteja huyo alimkabidhi Mlalamikaji pesa taslimu na akazihesabu na kujiridhisha kuwa zimetimia . Kabla mlalamikaji hajatuma pesa hizo mtuhumiwa aliomba arudishiwe pesa hizo kwanza ili afanye mawasiliano na anayemtumia  ambapo muda mfupi baadae mtuhumiwa alimuomba mlalamikaji atume pesa hiyo na kumkabidhi mlalamikaji pesa zenye ujazo kama ule wa awali,  bila ya kuwa na shaka yoyote alipokea bila kufanya uhakiki tena na kutuma pesa kiasi cha 900,000/ kwenda namba 0767 117552 na mtuhumiwa aliondoka.

ACP Sedoyeka alieleza kuwa baada ya mtuhumiwa huyo kuondoka mlalamikaji katika kuhakiki fedha hizo aligundua  kuwa pesa aliyopewa na Mteja kwa mara ya pili ilikuwa haijatimia na ilikuwa kiasi cha Tsh. 200,000/= ambapo zilikuwa zimechanganywa  noti za Tsh. 2,000/= nyingi kitendo ambacho kilimfanya mlalamikaji asitambue kuwa pesa zimeibwa kwa hiyo  badala ya 900,000/=  alibaini upungufu wa kiasi cha Tsh. 700,000/= . Baada ya kugundua wizi huo Mlalamikaji alitoa taarifa  Polisi ambapo Jeshi la Polisi kupitia Kitengo cha kufuatilia makosa ya mtandao walifanya ufuatiliaji wa tukio hilo ndipo tarehe 20.06.2016 kikosi kutoka Makao makuu kilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao wakiwa Jijini Dar es salaam ambapo katika mahojiano walikiri kutenda kosa hilo na taratibu zinafanyika ili waweze kufikishwa mahakamani.

Kisha  ACP Sedoyeka akaelezea  mbinu waliyoitumia watuhumiwa kuwa ni kuweka vitita  viwili vya pesa ambavyo vinakuwa na viwango tofauti lakini vina ujazo sawa na wanapofika katika maduka ya M – pesa  huonyesha kitita cha pesa kilicho sahihi  ambapo muamala unapokamilika tu huomba kubadilisha kitita na kutoa kitita mabacho kina kiwango kidogo tu cha pesa.

Kamanda Sedoyeka hakusita kutoa wito  kwa kuwataka  wananchi wote kuwa  makini na utapeli wa namna hii na wanatakiwa kuhakiki pesa za wateja wao kabla hawajafanya miamala ya kipesa na kuongeza kuwa kwa vile watuhumiwa wapo katika Kituo cha Polisi Singida,  wananchi waliotapeliwa/walioibiwa kwa njia ya mtandao wafike katika kituo hicho ili kuweza kuwatambua.

No comments