Mauaji ya
mfanyabiashara Singida. Jeshi la Polisi kufanya msako mkali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Debora Magiligimba akiongea na waandishi wa Habari Ofisini kwake leo asubuhi.
Na Sylvester Richard.
Singida.
Jeshi la Polisi
Mkoani Singida linaendesha msako mkali wa
kumsaka/kuwasaka watuhumiwa waliofanya mauaji ya mfanyabiashara ajulikanaye kwa jina la
Simon Charles, (49), mkazi wa Itungukia Manispaa ya Singida.
Akiongea na
waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishina
Msaidizi wa Polisi (ACP) Debora Magiligimba ameeleza kuwa tukio hilo la mauaji
lilitokea siku ya tarehe 20.04.2017 majira ya saa 3:30 usiku huko katika maeneo
ya
Stendi ya zamani, Kata ya Majengo, Tarafa ya Mungumaji, Wilaya na Mkoa
wa Singida.
Hata hivyo Kamanda
Magiligimba ameeleza kuwa mbinu waliyoitumia watuhumiwa hao ni kujificha
pembezoni mwa gari la mfanyabiashara huyo lenye Namba T.483 CJB aina ya Noah alilokuwa ameliegesha hatua chache toka katika
duka lake la madawa ya Binadamu lililopo katika eneo la Stendi ya zamani ambapo
alipotaka kupanda gari ili aondoke alipigwa risasi na watuhumiwa hao ambao walitorokea kusikojulikana.
Kamanda amesema
kuwa chanzo cha tukio hilo bado hakijajulikana na uchunguzi wa kina unaendelea ili kubaini nini
chanzo hasa na kueleza kuwa Mwili wa
Marehemu ulipelekwa katika Hospitali ya Mkoa Singida kwa uchunguzi wa Daktari
kabla ya kukabidhiwa kwa ndugu kwa hatua za mazishi.
Magiligimba ametoa wito kwa Wananchi wote wa
Mkoa wa Singida kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa
zitakazosaidia kuwakamata watuhumiwa wa tukio hilo na kuwafikisha Mahakamani ili kudhibiti
vitendo vya uhalifu kama huo na kuwataka wafanyabiashara kuweka walinzi katika
maeneo yao ya biashara ili kujihakikishi usalama katika maeneo yao ya biashara.
Kwa habari, Matangazo, Picha, Maoni na Ushauri. Wasiliana nasi kwa anwani zifuatazo
E - mail - sylvestermac87@gmail.com
- machibya.richard@yahoo.com
Simu No. - 0768 367 454 / 0652 683 063
Facebook Machibya Richard
No comments