MADAKTARI BINGWA WABAINI WAGONJWA ZAIDI YA 460 WA MOYO SONGWE
MADAKTARI BINGWA WABAINI WAGONJWA ZAIDI YA 460 WA MOYO SONGWE
Wagonjwa 467 wenye
matatizo ya moyo wamebainishwa na kupatiwa huduma ya ushauri na matibabu kutoka
kwa madaktari bingwa waliotoa huduma kwenye kambi maalumu ya siku 4 katika Hospitali ya Viwawa-Mbozi Mkoani Songwe.
Timu ya Madaktari
Bingwa na wauguzi 5 wameeleza kuwa wagonjwa 18 kati ya hao waliowahudumia
wamepewa rufaa ya kufika Hospitali za Rufaa kwa ajili ya matibabu Zaidi.
Daktari Bingwa wa
Magonjwa ya Moyo George Lyego Longopa Kutoka Taasisi ya Magonjwa ya Moyo ya
Jakaya Kikwete amesema wameanza matibabu siku ya Jumanne na kila Daktari
amekuwa akiona zaidi ya wagonjwa 60 kutokana na hamasa ya wagonjwa waliojitokeza
kupata matibabu ya magonjwa ya moyo.
“Tumeona wagonjwa wengi na tumeamini kuwa
Songwe tatizo la Magonjwa ya moyo bado ni kubwa, wagonjwa wengi wamekutwa na
matatizo ya shinikizo la damu, moyo kushindwa kufanya kazi vizuri pamoja na matatizo
ya mishipa ya damu kuziba”, amesema Dkt Longopa.
Afisa Muuguzi Kutoka
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Flora Kasembe ameeleza kuwa mtindo wa maisha
ya wananchi wa Songwe unaweza kuwa ni chanzo cha magonjwa ya moyo hasa kutokana
na uwepo vyakula vingi lakini wananchi hawali mlo kamili.
“tumekuwa tukitoa elimu ya kuzingatia mlo kamili ili hivi vyakula vingi
vilivyopo huku visaidie kuimarisha afya na sio waishie kuuza tu bila wao
kutumia, pia wananchi wajenge mazoea ya kufanya mazoezi na endapo watabainika
na matatizo na wakaanzishiwa dawa wazitumie kwa usahihi wasiache”. Kasembe amefafanua.
Baadhi ya wagonjwa
waliohudhuria kupata matibabu ya moyo wameishukuru Serikali kwa kusogeza huduma
karibu na utaratibu huo ufanyike mara kwa mara ili wananchi wengi wapate huduma
ya madaktari bingwa.
Brigita Haule ambaye
amepata matibabu ya moyo ameeleza kunufaika na huduma hiyo kwani hakuwa
akifahamu kama ana tatizo la moyo mpaka alipofika katika huduma hiyo.
“Wengi tunajiamini ni
wazima kwa kuwa hatusikia kuumwa sana ila tunatembea na magonjwa mbalimbali
ambayo tunakuja kuyafahamu yakiwa katika hali mbaya, mimi pia sikufahamu kama
nina tatizo hivyo nawashauri wote tuwe na utaratibu wa kupima afya zetu”,
amefafanua Bi Haule.
Kwa upande wake Kaimu
Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt Kheri Kagya amesema utaratibu wa kuwaalika madaktari
bingwa wa moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete uliangaliwa na uongozi
wa Mkoa baada ya kubaini kuwa kuna wagonjwa 210 wa moyo.
Dkt Kagya ameongeza
kuwa wagonjwa waliojitokeza wamekuwa wengi kuliko matarajio ya awali huku
akieleza kuwa hayo ni mafanikio kwakuwa wameweza kuwabaini wagonjwa ambao
hawakutambulika hapo awali.
Daktari Bingwa wa
Magonjwa ya Moyo George Lyego Longopa Kutoka Taasisi ya Magonjwa ya Moyo ya
Jakaya Kikwete akichukua maelezo ya mgonjwa wa moyo katika hospitali ya
Vwawa-Mbozi.
Afisa Muuguzi Kutoka
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Flora Kasembe akimpima shiniko la damu
mwandishi wa habari Manuel Kaminyoge katika hospitali ya Vwawa-Mbozi,
Baadhi ya wagonjwa
wakisoma kipeperushi kinachoeleza masuala ya lishe wakati wakisubiri kupata huduma
ya madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya
Kikwete katika hospitali ya Vwawa-Mbozi.
Kama una Habari, matangazo, Picha, Maoni au ushauri tuma kwa kupitia anwani zifuatazo;
E- mail. -sylvestermac87@gmail.com
-machibya.richard@yahoo.com
Sim No. 0768367454/0652683063
Namba yetu ya WhatsApp 0629 655814
Facebook - machibya richard.
No comments