Vikundi vya vijana vilivyosajiliwa vyaalikwa kufika Ofisi ya maendeleo ya Jamii Katika Manispaa ya Singida.
Vikundi vya vijana vilivyosajiliwa vyaalikwa kufika Ofisi ya maendeleo ya Jamii Katika Manispaa ya Singida.
HALMASHAURI Manispaa ya Singida imealika vikundi vya vijana vilivyosajiliwa kufika ofisi ya maendeleo ya jamii kupata msaada wa kuandikiwa ‘andiko’,kwa ajili ya kuombea fedha kwa wafadhili mbalimbali kuendeshea miradi au shughuli zao za ujasiriamali kwa ufanisi.
Mwaliko huo umetolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na Afisa maendeleo ya jamii Hanna Churi wakati akifunga mafunzo mbalimbali yakiwemo ya ujasiriamali wenye tija. Mafunzo hayo yamefadhiliwa na shirika la UK. Aid chini ya mradi wa Girls Educhation Challenges Window 2 (GECT 2). Unatekelezwa katika manispaa ya Singida na Wilaya ya Manyoni.
Amesema pamoja na kusaidiwa msaada wa kuandikiwa andiko la mradi, watapata fursa ya kupewa elimu mbalimbali ikiwemo namna bora ya kuanzisha shughuli za ujasiriamali.
“Tutavielimisha namna na mbinu ya kuanzisha biashara endelevu au yenye tija, fursa za kupata mikopo na upatikanaji wa masoko.Pia fursa ya kunufaika na mikopo inayotolewa na Halmashauri kutoka mapato yake ya ndani”,alisema Churi.
Akifafanua,afisa huyo,alisema kwa sasa mikopo kutoka Halmashuri za Wilaya na Manispaa, haina riba yo yote. Mikopo husika inarudishwa bila kutozwa riba ya aina yo yote.
Aidha,Churi alisema kuwa huko nyuma vikundi vilivyosajiliwa vilikuwa vinapatiwa mikopo kwa ajili ya kuendeshea mradi/shughuli ya aina moja tu.Kwa sasa kila mwanachama wa kikundi husika, anaruhusiwa kufanya shughuli anayoichangua binafsi.
Katika hatua nyingine,Afisa huyo alisema vile vile ofisi yake inatoa msaada wa kuviunganisha vikundi na taasisi mbalimbali za kifedha,ili iwe rahisi kukopa.
“Kwa kifupi niwaambie tu ninyi vijana,kujiunga kwenye vikundi na mkavisajili, kuna faida nyingi mno.Serikali,wafadhili au wadau mbalimbali,hawawezi kusaidia kijana mmoja moja.Sharti lao ni vijana kuanzisha vikundi na kuvisajili. Kwa njia hiyo mtatambulika kisheria na mtakuwa mmejijengea mazingira mazuri ya kukopesheka”alisema.
Mwongozaji wa wanafunzi kutoka shule ya sekondari Manyoni, Bahati Jonas amesema kupitia mafunzo hayo, wamejengewa uwezo zaidi wa namna bora ya kufikia malengo kielimu.
Naye mkazi wa manispaa ya Singida ambaye hupo nje ya shule Devota Beda, alisema kupitia mafunzo hayo amejengewa uwezo juu ya ulinzi wa mtoto.
Awali mratibu wa mradi huo, Lilian Walter amesema lengo la mradi huo ni kuwasaidia na kuwahamasisha wasichana waliopo ndani na nje ya shule, kujitambua.
MWISHO.
Afisa maendeleo ya jamii manispaa ya Singida (kushoto) Hanna Churi,akikabidhi simu ya kiganjani mwongozaji wanafunzi katika shule za sekondari wilaya ya Manyoni. Simu hizo zimetolewa na shirika la UK Aid,kwa ajili ya mtandao wa Waongozaji wa wanafunzi katika shule za sekondari za manispaa ya Singida na wilaya ya Manyoni. Picha na Nathaniel Limu.
Afisa maendeleo ya jamii manispaa ya Singida Hanna Churi,akitoa nasaha zake wakati akifunga mafunzo yakiwemo ujasiriamali yaliyohudhuriwa na waongozaji wa wanafunzi wa shule za sekondari manispaa ya Singida na wilaya ya Manyoni.Mafunzo hayo yamefadhiliwa na shirika la UK Aid ambayo yanatekelezwa kupitia mradi wa Girls Education Challenges (GECT 2). Picha na Nathaniel Limu.
Afisa maendeleo ya jamii manispaa ya Singida (katikati walioketi) Hanna Churi,akiwa kwenye picha ya pamoja na Waongozaji 56 (walionyanyua juu simu) wa wanafunzi wa Shule za Sekondari katika Manispaa hiyo na Wilaya ya Manyoni.Waongozaji hao walihudhuria mafunzo ya kujengewa uwezo zaidi kwa lengo la kutoa elimu mbalimbali mashuleni ikiwemo elimu itakayowasaidia kufikia malengo yao kielimu.Wa kwanza kushoto ni mratibu wa mradi wa GECT 2,Lilian Walther na kulia ni Mwongazaji kiongozi kutoka Manyoni Sekondari,Bahati Jonas.Picha na Nathaniel Limu.
Kama una Habari, matangazo, Picha, Maoni au ushauri tuma kwa kupitia anwani zifuatazo;
E- mail. -sylvestermac87@gmail.com
-machibya.richard@yahoo.com
Sim No. 0768367454WhatsApp/0652683063
Facebook - machibya richard.
No comments