Breaking News



JESHI LA POLISI TANZANIA
OFISI YA KAMANDA WA POLISI “M” SINGIDA

23.05.2016
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
(PRESS RELEASE)

MATUKIO YA AJALI NA UVUNJAJI
Mnamo tarehe 22.05.2016 matukio ya ajali mbili na moja la uvunjaji yametokea Mkoani Singida  katika  maeneo na nyakati tofauti.

Tukio la  kwanza   ni ajali ya magari mawili kugongana na kusababisha kifo na majeruhi ambayo imetokea majira ya saa 11: 00 jioni huko katika eneo la Mlima Saranda, Kata ya Chikuyu, Wilayani Manyoni ambapo Dereva aitwaye Bakari s/o Ally (32), mmatumbi akiendesha gari lenye  namba T. 209 ASQ aina ya FUSO akiteremka Mlima Saranda akitokea Igunga – Dar es salaam alishindwa kulimudu gari na kugongana na Gari lenye namba T. 439 DFL DRAGON BUS linalomilikiwa na Kampuni ya LEO LUXURY COACH  likiendeshwa na Dereva aitwaye Ridhaa s/o Mohamed , (36), Mpogoro na mkazi wa Dar es salaam akitokea Dar es salaam - Mwanza.

Aidha katika ajali hiyo Dereva wa gari namba T. 209 ASQ aina ya FUSO Bakari s/o Ally alifariki dunia papo hapo na kusababisha majeruhi kwa abiria mmoja wa FUSO  hilo aitwaye Richard s/o Dominick, (40), Mjaluo, Mfanyabiashara na mkazi wa Kibaha ambaye amevunjika mkono wa kulia.

Uchunguzi wa awali wa Polisi umebaini chanzo cha ajali hiyo kuwa ni gari lenye  namba T. 209 ASQ aina ya FUSO kufeli breki. Majeruhi amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni kwa matibabu, halikadhalika mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitalini hapo ukisubiri taratibu za mazishi ambapo hakuna mtu/watu wanaoshikiliwa na Polisi kuhusiana na ajali hiyo.

Tukio la Pili   ni la ajali  ya Gari kumgonga mwendesha pikipiki na kusababisha kifo ambayo imetokea majira ya saa 2:00 usiku huko katika Mtaa wa Mjengo Manyoni Mjni, Kata, Tarafa na Wilaya ya Manyoni ambapo Dereva aitwaye Noel s/o Emanueli, (24), Mchaga na Mkazi wa Arusha Mjini akiendesha gari namba T.599 BDD/T.434 SCANIA SEMI TREILER akitokea Arusha – Mafinga alimgonga mwendesha pikipiki aitwaye Riziki s/o Samsoni ,(26), Mgogo  Dereva wa pikipiki na kusababisha kifo chake papo hapo.

Aidha chanzo cha ajali hiyo kimebainika kuwa ni uzembe wa Dereva wa Gari ambaye alikuwa akilipita gari lililokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari kwa watumiaji wengine wa barabara hivyo kumgonga mwendesha pikipiki huyo aliyekuwa akiendesha pikipiki yenye namba MC 907 ATD aina ya FEKON na kupelekea kifo chake papo hapo.

Kuhusiana na ajali hiyo Jeshi la Polisi linamshikilia dereva wa gari Noel s/o Emanueli kwa uchunguzi na baada ya uchunguzi kukamilika atafikishwa Mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili. Mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa kwa ndugu kwa hatua za mazishi.

Jeshi la Polisi linatoa wito kwa madereva wote wa vyombo vya usafiri kuendesha vyombo vyao kwa kuzingitia sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani na pia wanatakiwa kuvikagua na kuvifanyia matengenezo vyombo vyao kabla ya kuanza safari ili kuepusha ajali zisizokua na ulazima.

Tukio lingine   ni la kuvunja nyumba mchana na kuiba ambalo lilitokea majira ya saa 12:00 jioni nyumbani kwa Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Mh. Cosmas s/o Pascal, () ambapo alipigiwa simu na Mlinzi wa nyumba yake aitwaye Said s/o Abdalah, (49), Mnyaturu, na kuelezwa kuwa nyumba yake imevujwa na vitu mbalimbali vyenye thamani ambayo bado haijajulikana vimeibwa.

Kuhusiana  na na tukio hilo , Jeshi la Polisi linamshikilia mlinzi  Said s/o Abdalah  kwa mahojiano ili kulisaidia jeshi hilo katika kuwapata wahusika wa tukio hilo. Pia jeshi la Polisi linatoa wito kwa raia wema kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kuwakamata watu waliohusika na tuko hilo ili wakamatwe na sheria ichukue mkondo wake.

Imetolewa na; 
Thobias G. Sedoyeke - ACP   
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida.

No comments