Breaking News



MWADUI FC YA  SHINYANGA YASHINDWA KUTAMBA MBELE YA SINGIDA UNITED


 

Na Sylvester Richard.
 
SINGIDA
Timu ya Mpira wa miguu Mwadui FC ya Mkoani Shinyanga inayoshiriki ligi kuu ya Vodacom msimu huu imeshindwa kuibuka na ushindi katika mchezo wa kupimana nguvu na Timu ya Singida United timu ambayo inawakilisha Mkoa wa Singida katika ligi daraja la kwanza kwa msimu unaonza hivi karibuni.

Mchezo huo uliochezwa katika uwanja wa Namfua Manispaa ya Singida ukichezeshwa na Mwamuzi Shabani Msangi  Kutoka Singida ulichezwa majira ya saa 10:30 jioni siku ya tarehe 20.08.2016 ambapo hadi kipenga cha mwisho timu zote zilikuwa zimefungana goli moja moja.

Aidha timu ya Singida United ndiyo timu ya kwanza kufunga ambapo mchezaji wake Elinywesi Sumbi aliweza kupenya katika Ngome ya Mwadui  FC hivyo kufanikiwa kuzifumania nyavu na kuipatia timu yake goli katika dakika ya 13 ya mchezo huo goli ambalo lilidumu hadi kipindi cha mapumziko.

Hata hivyo kipindi cha pili cha mchezo huo kilianza huku mpambano ukizidi kuwa mkali zaidi kwa timu zote ili kupata magoli zaidi ambapo kunako dakika ya 87 ya mchezo huo beki wa timu ya Singida United alifanya madhambi ndani ya kumi na nane na hivyo mwamuzi wa mchezo huo Shabani Msangi kuamuru ipigwe penalt, penalt ambayo ilipigwa na Mshambuliaji wa Mwadui FC Hassan Kabunda na kuipatia timu yake bao la kusawazisha.

Akiongea na waandishi wa habari muda mfupi tu baada ya pambano hilo, Kocha wa Mwadui FC Jamhuri Kuweru @ Julio alimpongeza Kocha wa  timu ya Singida United kwa kuwaandaa vizuri vijana wake hatimaye katoka sare dhidi ya timu yake huku akieleza kuwa uwanja haufai unahitaji marekebisho. Aliwataka waamuzi kufanya kazi kwa kutenda haki bila upendeleo ili kuzijengea timu uwezo wake kuliko kuzibeba kwani kufanya hivyo kunaua vipaji.

Naye Kocha wa timu ya Singida United Felix Minziro alieleza kuwa timu yake iko vizuri kutokana na maandalizi mazuri pamoja na kuwa na timu yenye mchanganyiko wa wachezaji wachanga na wazoefu hali ambayo aliitaja kuwa imeleta matokeo mazuri kwake. Alisema kupitia mchezo huo yapo aliyojifunza na atayafanyia kazi na atahitaji michezo mingine zaidi kama hiyo ili kukinoa kikundi chake.






1 comment: