IKUNGI, MFUKO WA ELIMU UTABORESHA ELIMU HASA KWA KUJENGA MAABARA.
Afisa Tawala Mkao wa Singida Dkt Angelina Mageni Lutambi amewapongeza wananchi
wa Ikungi Mkoani Singida kwa kuupokea mfuko wa elimu ambao una mpango wa miaka mitatu yaani
2017-2020 wa kukusanya zaidi ya bilioni tatu zinazohitajika kutatua changamoto mbalimbali za elimu Wilayani humo.
Dkt. Lutambi ametoa pongezi hizo wakati akiwa Mgeni rasmi wa
ufunguzi wa Ligi ya mpira wa miguu ambayo ina lengo la kuutambulisha kwa wananchi na wadau mbalimbali
mfuko huo wa elimu ili wahamasike kuuchangia huku akiwa amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi.
Dkt Lutambi amesema
mfuko huo utaboresha elimu hasa ujenzi wa maabara ambazo ni msingi wa maendeleo
ya sayansi ambapo bila kufanya vizuri katika sayansi Wilaya hiyo haitaweza
kujikomboa katika kuelekea uchumi wa viwanda ambao utaichangia Nchi kufikia uchumi wa kati.
“Ukombozi wa Nchi yoyote
bila sayansi haiwezekani, Ikungi mkiboresha mazingira ya hawa wanasayansi
wanafunzi mnatengeneza jamii ya wanasayansi ambao wataikomboa Wilaya yetu kwa
kuweka ubunifu kwenye viwanda ambavyo hukuza uchumi kwa haraka”, amesisitiza.
Ameongeza kuwa Ligi
hiyo isaidie kuwaunganisha wananchi hao na kuchangamkia katika kuchangia
maendeleo ya elimu Wilayani humo, aidha ameitaka Halmashauri kusimamia mfuko
huo kwa umakini ili uweze kutekeleza majukumu yaliyotarajiwa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu ametoa rai kwa Wanasiasa hasa wasomi
na wale wenye ushawishi mkubwa na kuwataka kuacha kulalamika na kutoa kauli
ambazo hazitawasaidia wananchi katika kuwatatulia matatizo na kero zao bali
waungane na Serikali katika juhudi zinazoonekana kuleta maendeleo.
Mtaturu amesema baadhi
ya wanasiasa maarufu wamekuwa wakitumia muda mwingi kueleza matatizo na kero za
wananchi bila ya kuonyesha suluhisho au kusaidia kutatua kero hizo jambo ambalo
halimsaidii mwananchi kwa namna yoyote.
“Baadhi ya Wanasiasa
utawaona mstari wa mbele kutajataja kero za wananchi wanapokuwa majukwaani
wakati hawatoi mchango wowote wa kutatua kero hizo au hata kueleza mapendekezo
ya nini kifanyike, acheni kufanya hivyo kwakuwa mna watonesha vidonda wananchi,
kusema sema hakusaidii, onyesha njia ya kumsaidia mwananchi kama ambavyo sisi
tunafanya leo katika sekta ya elimu”, amesema Mtaturu.
Amesema Sekta ya
elimu Wilayani humo inakabiliwa na uhaba wa nyumba za walimu, vyumba vya
madarasa na maabara.
Mtaturu amesema kati
ya mahitaji ya maabara 90 wilayani humo, zipo maabara nne tu na kwa kuanzia
mfuko huo umeweka malengo ya kuhamasisha wananchi kufyatua tofali elfu kumi kwa
kila Kata ili ziweze kutatua changamoto hiyo.
Ameongeza kwa
kuwapongeza wananchi, viongozi na madiwani waliojitokeza kuchangia mfuko huo
ambapo yeye amechangia mifuko mia moja ya simenti, Wadau na wananchi walitoa mifuko
194 ya simenti, fedha taslimu laki nane, ahadi milioni moja laki tisa, mchanga ‘trip’
tano na moramu.
“Nawashukuru sana
madiwani wa Ikungi na wananchi kwakweli tumeanza vizuri na nina imani mfuko huu
wa elimu utasaidia kupunguza changamoto za sekta ya elimu wilayani humu,
tunaendelea kukaribisha wadau mbalimbali, lakini pia wananchi msisite kama una
mchanga leta, una siment hata maji tu ni mchango pia tusikariri mchango lazima
ni fedha”, ameongeza.
Naye Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Singida ACP Debora Daudi Magiligimba amesema michezo huleta
amani na kusaidia katika kuhamasisha maendeleo hivyo basi ligi hiyo isaidie
kuhamasisha kwa amani uchangiaji wa mfuko huo.
Wakati huo huo ACP
Magiligimba amewapongeza wananchi wa Ikungi na Mkoa wa Singida kwa kushirikiana
na Jeshi la Polisi katika kupunguza wahalifu na uhalifu.
Amesema uhalifu
umepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na ushirikiano wanaoupata kutoka kwa
wananchi licha ya uhalifu wa ubakaji ukionekana kuongezeka hivyo amewataka
wananchi kuendela kutoa ushirikiano ili ubakaji uishe.
ACP Magiligimba
amewataka wananfunzi kuacha vitendo vya ngono na vijana kuacha matumizi ya
madawa ya kulevya kwakuwa yote hayo huharibu maisha yao bali wakazane katika
masomo na michezo.
Ligi ya mpira wa
miguu Wilayani Ikungi yenye lengo la kuhamasisha wananchi na wadau kuchangia
mfuko wa elimu imeanza rasmi jana na inatarajiwa kuhitimishwa mwezi Septemba
ambapo zaidi ya timu 69 zitashiriki.
Mkuu wa Wilaya ya
Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu akiwania mpira katika mechi ya ufunguzi wa Ligi
ya elimu yenye lengo la kutunisha mfuko wa elimu wilayani humo, mechi kati ya
madiwani wa Halmashauri ya Ikungi na Manispaa ya Singida ilizindua ligi hiyo na
kutoka sare ya bila bila.
Katibu Tawala Mkoa wa
Singida Dkt Angelina Mageni Lutambi akifyatua tofali wakati wa uzinduzi wa Ligi
ya elimu yenye lengo la kutunisha mfuko wa elimu wilayani humo, Matofali elfu
kumi yanatarajiwa kufyatuliwa kwa kila kata.
Mkuu wa Wilaya ya
Ikungi Miraji Mtaturu akifyatua tofali wakati wa uzinduzi wa Ligi ya elimu yenye
lengo la kutunisha mfuko wa elimu wilayani humo, Matofali elfu kumi
yanatarajiwa kufyatuliwa kwa kila kata.
Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Singida ACP Debora D. Magiligimba akizungumza wakati wa uzinduzi wa Ligi
ya elimu yenye lengo la kutunisha mfuko wa elimu wilayani humo, Matofali elfu
kumi yanatarajiwa kufyatuliwa kwa kila kata.
Sehemu ya mchango ya
simenti kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu pamoja na wadau
mbalimbali ambapo Matofali elfu kumi yanatarajiwa kufyatuliwa kwa kila kata ili
kutunisha mfuko wa elimu Wilayani humo wenye lengo la kutatua baadhi ya changamoto
ya ukosefu wa maabara na vyumba vya madarasa.
Katibu Tawala Mkoa wa
Singida Dkt Angelina Mageni Lutambi akimkabidhi bahasha yenye shilingi laki mmoja
kati ya wanafunzi 16 wa Sekondari ya Ikungi waliopata ufaulu wa daraja la kwanza
katika matokeo ya kidato cha sita kama sehemu ya kuhamasisha wanafunzi na
walimu kufanya vizuri, aidha wanafunzi hao walipatiwa shilingi laki moja kila mmoja huku
walimu wakipatiwa motisha ya shilingi milioni moja.
Baadhi ya wananchi wakijitolea
kufyatua tofali ambapo Matofali elfu kumi yanatarajiwa kufyatuliwa kwa kila
kata ili kutunisha mfuko wa elimu Wilayani humo wenye lengo la kutatua baadhi
ya changamoto ya ukosefu wa maabara na vyumba vya madarasa.
Kama una Habari., Matangazo, Picha, Maoni na ushauri , tuma kupitia anwani zifuatazo;
E-mail sylvestermac87@gmail.com/machibya.richard@yahoo.com
Sim no . 0768367454/0652683063 . WhatsApp 0629655814
E-mail sylvestermac87@gmail.com/machibya.richard@yahoo.com
Sim no . 0768367454/0652683063 . WhatsApp 0629655814
No comments