WAKULIMA KUPATA MBEGU BORA YA ALIZETI MKOANI SINGIDA.
SINGIDA
Wakulima wa zao la
alizeti Mkoani Singida wamepata uhakika wa mbegu bora ya alizeti ambayo itawasaidia
kuzalisha kibiashara tofauti na hapo awali walipokuwa wakipata mbegu zisiso na
uhakika wa mavuno mazuri.
Mwenyekiti wa chama
cha Wakulima wa Alizeti Mkoa wa Singida Athumani Sima amesema hayo mapema leo
katika mkutano wa wadau wa kilimo cha alizeti ulioandaliwa na mradi wa Faida
Mali kupitia Shirika la AMDT ambalo limejikita katika kusaidia wakulima wa zao
hilo kupata mbegu bora.
Sima amesema hapo
awali wakulima walikuwa wakinunua mbegu kwa wauzaji ambao sio waaminifu na
hivyo kutovuna vizuri kutokana na mbegu hizo kuota vibaya na kutoa alizeti
kidogo.
Amesema mradi wa
Faida Mali umewahakikishia kuwasaidia upatikanaji wa mbegu bora na ya kisasa na
hivyo kukifanya kilimo cha alizeti kuwa kama biashara nyingine ambazo zina
faida kubwa.
“Hawa Faida Mali sisi
tunawaamini kwakuwa wamekuwa wakishirikiana na serikali hivyo watatusaidia
katika kupata mbegu bora, tulikuwa tunaumizwa na wauzaji wengine akikuuzia
mbegu inaota hapa, pale haioti matokeo yake unapata hasara” amesema na kuongeza
kuwa,
“Mkulima akipata
Mbegu bora hiyo ni hatua ya kwanza ya mafanikio, kwakweli baadhi yetu tulianza
kukata tamaa kwa kuona tunapata hasara tu, unalima alizeti miaka mingi huoni
faida kubwa kama ambavyo unatarajia, lakini mradi huu umetuonyesha njia ya
mafanikio, nawaomba wakulima wengine waweze kujiunga katika vikundi ili waweze
kufikiwa na mradi huu au miradi mingine”, amesisitiza.
Naye Mkulima wa alizeti
Kutoka kata ya Kinampundu Wilaya ya Mkalama Samwel Laida amesema utaratibu wa
kununua alizeti kwa magunia ya lumbesa badala ya vipimo vya mizani unawapunja
wakulima na kuwafanya warudi nyuma kiuchumi.
Laida amesema
wanunuzi wa alizeti wanapakia alizeti katika magunia na kushindilia ambapo
kipimo hicho sio sahihi na hakilengi kumwinua mkulima hivyo basi mradi wa Faida
Mali unapowasaidia kutafuta masoko uangalie na vipimo vinavyotumika katika
kununua zao hilo.
Kwa upande wake
Meneja wa Mradi wa Faida Mali Mkoa wa Singida Christopher Mkondya amesema ili
wakulima wazalishe kibiashara watawasaidia kupata mbegu bora na ya kisasa, kupata
huduma mbalimbali za ugani, masoko na kuwaunganisha wakulima hao na huduma za
kifedha.
Mkondya amesema kwa
kushirikia na Autainsurance watawasaidia wakulima kupata elimu ya faida za bima
na hivyo watakata bima ya mazao yao ili wakipata majanga yoyote kama vile moto,
mafuriko, au mbegu kutoota wataweza kufidiwa na kuepuka hasara.
Ameongeza kuwa
kupitia watoa huduma wao ambao ni Ersoko wamejipanga kutoa elimu kwa wakulima
hasa kwa kuwatumia ujumbe mfupi wa maneno ambapo mkulima atapata taariza zote
za kilimo cha alizeti kulingana na eneo alipo kwa kumuelekeza mbinu za kulima
kisasa, muda wa kupanda, aina ya mbolea na taarifa za masoko ya mazao yake.
Mwenyekiti wa chama
cha Wakulima wa Alizeti Mkoa wa Singida Athumani Sima akisisitiza jambo katika
kikao cha wadau wa kilimo cha alizeti, kilichoandaliwa na Mradi wa Faida Mali.
Meneja wa Mradi wa
Faida Mali Mkoa wa Singida Christopher Mkondya akiandika maoni ya wakulima wa
alizeti wakati wa majadiliano katika kikao cha wadau wa kilimo cha alizeti.
Baadhi ya wakulima wa
alizeti wakiandika baadhi ya maelekezo, mapendekezo na maoni yaliyotolewa katika
kikao cha wadau wa kilimo cha alizeti, kilichoandaliwa na Mradi wa Faida Mali.
Mkulima wa alizeti
Kutoka kata ya Kinampundu Wilaya ya Mkalama Samwel Laida akifafanua jambo katika
kikao cha wadau wa kilimo cha alizeti, kilichoandaliwa na Mradi wa Faida Mali.
Mkurugenzi wa Faida
Mali Mkoa wa Singida Tom Silayo akiwaelezea wakulima wa alizeti mambo ambayo
mradi huo utayatekeleza.
Afisa Kilimo
Sekretarieti ya Mkoa wa Singida Mashaka Mlangi na Afisa Maendeleo ya Jamii
Patrick Kassango wakichukua maoni ya wakulima walioudhuria kikao cha wadau wa
kilimo cha alizeti kwa ajili ya utekelezaji na ufuatiliaji.
Kama una Habari., Matangazo, Picha, Maoni na ushauri , tuma kupitia anwani zifuatazo;
E-mail sylvestermac87@gmail.com/machibya.richard@yahoo.com
Sim no . 0768367454/0652683063 . WhatsApp 0629655814
E-mail sylvestermac87@gmail.com/machibya.richard@yahoo.com
Sim no . 0768367454/0652683063 . WhatsApp 0629655814
No comments