Breaking News

Jeshi la Polisi lakanusha taarifa za Askari wa Jeshi la Polisi kuhusishwa na muendelezo wa tukio la kujeruhiwa kwa risasi kwa Mhe. Tundu Lissu (MB).


Jeshi la Polisi lakanusha taarifa za Askari wa Jeshi la Polisi kuhusishwa na muendelezo wa tukio la kujeruhiwa kwa risasi kwa Mhe. Tundu Lissu (MB).

Katika siku za karibuni kumejitokeza vitendo vya baadhi ya watu kutumia majina ama picha za watu na kuwahusisha na matukio ya kihalifu au matukio yanayohusiana na uhalifu kwa lengo la kujipatia umaarufu, kuwachafua watu hao au kuwakosanisha na jamii inayowazunguka.
 
Kutokana na vitendo hivyo ACP Barnabas David Mwakalukwa ambaye ni Msemaji wa Jeshi la Polisi Makao Makuu emekutana na Waandishi wa Habari na kueleeza kuwa Mnamo tarehe 11.09.2017 kupitia mitandao ya kijamii kulisambaa picha ya askari wa Jeshi la Polisi akihusishwa na muendelezo wa tukio la kujeruhiwa kwa risasi kwa Mhe. Tundu Lissu (MB) ambapo taarifa hiyo ilimtambulisha askari huyo kuwa ni kachero wa Kitengo cha Interpol na kwamba yupo jijini Nairobi nchini Kenya akifuatilia taarifa za Mhe. Lissu.

ACP Mwakalukwa ameeleza kuwa Jeshi la Polisi linapenda kukanusha taarifa hizo kuwa si za kweli  na ni za uongo zenye lengo la kumchafua askari huyo na Jeshi la Polisi kwa ujumla na kuongeza kuwa Askari huyo hayupo Nairobi kama ilivyoenezwa na picha iliyotumika ilipigwa hapa nchini tarehe 07.01.2017 kwenye sherehe ya mahafali ya mtoto wa kaka yake.
 
Akiongea Kuhusiana na safari ya Nairobi,  ACP Mwakalukwa amesema askari huyo alikuwa Nchini Kenya kwa kozi ya kimafunzo kuanzia tarehe 04.09.2017 na kurejea tarehe 08.09.2017, huku Mhe. Lissu akipatwa na mkasa wa kujeruhiwa kwa risasi Tarehe 07.09.2017 na kusafirishwa kwenda Nairobi usiku wa kuamkia tarehe 08.09.2017.
 
Aidha Mwakalukwa amesisitiza na kusema kuwa Jeshi la Polisi linakemea vikali kitendo hiki chenye lengo la kumharibia maisha yake askari huyo, na linawataka wale wote waliohusika kusambaza au kutajwa katika taarifa hizo kuripoti kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa ajili ya mahojiano na kutoa onyo kwa wote wanaofikiri kuwa wanaweza kukaa na kupika habari ili waweze kuivuta jamii iwe upande wao na kuchafua upande wa serikali.
 
Akizungumzia suala la Mhe. Lissu ameeleza kuwa lipo chini ya uchunguzi ili kuwabaini wote waliohusika na tukio hili na hatimaye kuwafikisha mahakamani na kuwataka wananchi na wanasiasa wakaliacha Jeshi la Polisi liweze kufanya kazi yake bila kuliingilia ili kuweza kupata ukweli wa jambo hili.
 
Hata hivyo ACP Mwakalukwa ameitaka Jamii itambue kuwa Jeshi la Polisi linafanyakazi kwa mujibu wa Sheria, kanuni na taratibu za Nchi na kamwe halifanyi kazi kwa kuvizia na kueleza kuwa endapo mtu yeyote anahitaji taarifa, Jeshi la Polisi lina mifumo rasmi inayoliwezesha kupata taarifa linazozitaka kupitia uhusiano uliopo ndani na nje ya Nchi na kuongeza kuwa Jeshi la Polisi kupitia Kitengo cha upelelezi wa makosi ya mitandao (Cyber Crime Investigation Unit) linaendelea na uchunguzi ili kuwabaini wote waliohusika na kusambaa kwa taarifa hizi za uongo ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
 
Mwakalukwa ametoa rai kwa wananchi kuacha kutumia mitandao ya kijamii vibaya na badala yake mitandao hii itumike kwa ajili ya kuelimisha na kuihabarisha jamii juu ya masuala mbalimbali ya kimaendeleo.


Kama una Habari., Matangazo, Picha, Maoni na ushauri , tuma kupitia anwani zifuatazo;
E-mail sylvestermac87@gmail.com/machibya.richard@yahoo.com
Sim no . 0768367454/0652683063 . WhatsApp 0629655814


No comments