Breaking News

Watu wawili wadhaniwa kufariki dunia baada ya kufukiwa na mgodi Mkoani Singida


Watu wawili wadhaniwa kufariki dunia baada ya kufukiwa na mgodi Mkoani Singida.
Na Sylvester Richard.

SINGIDA
Watu wawili wanadhaniwa kufariki Dunia Mkoani Singida baada ya kufukiwa na udongo wa Mgodi wakati wakichimba madini.

Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake hii leo Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Mrakibu mwandamizi (SSP) Isaya K. Mbughi ameeleza kuwa tukio hilo lilitoke siku ya tarehe 09.09.2017 majira ya saa 7:47 usiku katika Kijiji cha Konkilangi, Kata ya Ntwike, Tarafa ya Shelui, Wilaya ya Iramba katika Mgodi ujulikanao kwa jina la Sekenke 1 katika  kitalu namba 1 ambapo maduara matano yanayomilikiwa na Marijan Ramadhani na Jakobo Ntobi yalititia na kusababisha majeruhi kwa wachimbaji 5 ambao waliwahi kuokolewa na wengine wawili wanadhaniwa kufariki dunia wakati juhudi za kuopoa miili yao zikiendelea.


Kaimu Kamanda amewataja Waliojeruhiwa katika ajali hiyo ambao tayari wameokolewa kuwa ni pamoja na;  Ayubu  Msengi, (34), mnyiramba, mkazi wa Ntwike ana jeraha kichwani na maumivu kiunoni, Mwita Salumu, (42), mnyiramba, mkazi wa Gumanga ana maumivu bega la kushoto na ubavu wa kushoto na Lazaro Edward, (28), mnyiramba, mkazi na mkulima wa Kiomboi Soweto ambaye anajeraha kichwani na maumivu shingoni.

Aliwataja majeruhi wengine kuwa ni Jeremi Idd, (41),mnyiramba, mkazi wa Kijiji cha Gumanga anamaumivu kiunoni na Jumanne Said, (24), mnyiramba na mkazi wa Mgongo anamaumivu kichwani na kusema  hali zao zinaendelea vizuri baada ya kupata matibabu katika  Hospitali ya Wilaya ya Iramba.

Hata hivyo SSP Mbughi amewataja  wachimbaji  wawili ambao ni Simon Odochi,@ Wa Mwanza, anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 26, Mkurya, na mkazi wa Mwanza na Kashinde Nkula anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 27, mkazi wa Kijiji cha Mangasu, Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga, wote wachimbaji wadogo wa madini  wanaosadikiwa kufariki dunia wakiwa bado wamefukiwa na kifusi ambapo Jeshi la Polisi kwa kusaidiana na wananchi linaendelea na juhudi za kuopoa miili yao kwa kutumia vifaa mbalimbali likiwemo gari maalumu (CATAPILLER).   

SSP Mbughi ameeleza kuwa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wataalam wa Migodi wanaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo hasa cha kutitia kwa migodi hiyo



Kaimu kamanda ametoa wito kwa wamiliki wa Migodi kuzingatia sheria za usalama wa Migodi. Pia ameatoa wito kwa mamlaka za ukaguzi wa Migodi kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuepusha ajali zisizo za lazima na kuongeza kuwa Jeshi la Polisi linawatafuta wamiliki wa Mgodi huo waliotoroka baada ya ajali hiyo. 

Kama una Habari., Matangazo, Picha, Maoni na ushauri , tuma kupitia anwani zifuatazo;
E-mail sylvestermac87@gmail.com/machibya.richard@yahoo.com
Sim no . 0768367454/0652683063 . WhatsApp 0629655814


No comments